Habari

Imewekwa: 12/08/2023

MAHAFALI YA 20 YA CHUO CHA TAIFA CHA HALI YA HEWA TAREHE 12/08/2023

MAHAFALI YA 20 YA CHUO CHA TAIFA CHA HALI YA HEWA  TAREHE 12/08/2023

Chuo cha Taifa Cha Hali ya Hewa kimefanya mahafali ya 20 yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa". Katika sherehe hizo za mahafali mgeni rasmi alikuwa ni Dkt.Makame Omary Makame ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Taifa cha Hali ya Hewa.

Katika hotuba yake mgeni rasmi aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuwezesha mafunzo katika chuo cha Hali ya Hewa

“Natoa pongezi nyingi kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kuwezesha mafunzo haya kufanyika na leo tunashuhudia mahafali ya wahitimu waliobobea kwenye masuala ya Hali ya Hewa kwa ngazi ya NTA Level 4, NTA Level 5 na NTA Level 6”. Alisema Dkt. Makame.

Pia,alitoa pongezi kwa kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt.Ladislaus Chang’a kwa kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa jopo la wanasayansi wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani (IPCC).

“Naomba tusimame na kupiga makofiishara ya kumpongeza kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Dkt.Ladislaus Chang’a kwa kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa jopo la wanasayansi wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani (IPCC) huu ni ushindi wa TMA,Tanzania na Afrika kwa ujumla” Alisema Dkt. Makame.

Aidha, Dkt. Makame alipongeza juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kupitia uongozi wa Chuo kwa kuanzisha Programu ya tehama“ICT” na kufanya ukarabati wa majengo ya chuo.

Dkt. Makame pia alielezea umuhimu wa Hali ya Hewa katika maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo,uvuvi,maji,uzalishaji Nishati,usafiri wa anga,majini na nchi kavu na kusema mafanikio ya shughuli hizi zote yanategemea sana taarifa za Hali ya Hewa.

Aidha Dkt.Makame alitoa rai kwa Wahitimu wote wakawe mabalozi wazuri katika kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa taarifa za Hali ya Hewa na kuzingatia tahadhari zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ili kusaidia wanannchi kuepuka madhara yatokanayo na maafa.

Mwisho, mgeni rasmi aliwapongeza wahitimu wote,wakufunzi na wafanyakazi wote wa Chuo pamoja na meneja wa Uwanja wa ndege Kigoma kwa kazi nzuri ya kuwaandaa wahitimu kwa kuwapatia ujuzi wa taaluma ya Hali ya Hewa na kuwahimiza kuzingatia maadili,kanuni na taratibu za kazi.

Mwisho napenda kumalizia kwa kusema, Mamlaka ya Hali ya Hewa bila UKIMWI inawezekana. Mkoa wa Kigoma bila UKIMWI inawezekana, na Tanzania nzima bila UKIMWI inawezekana”. Alisema Dkt. Makame.