Wasifu

Card image cap
Mkurungezi Mkuu
Dkt Agnes Lawrence Kijazi

Dkt. Agnes Kijazi ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu mwaka 2011. Dkt. Kijazi aliajiriwa na TMA mwaka 1988 na alianzia ngazi ya chini kabisa kama mtaalamu msaidizi wa hali ya hewa (Meteorological Assistant). Dkt. Kijazi pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO. Kwa upande mwingine Dkt. Kijazi ni Mjumbe na Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Umoja wa Mataifa (UN) mahsusi kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), 10 Member Group in support of Technology Facilitation Mechanism (TFM)". Pia Dkt. Kijazi kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za Kusini mwa Afrika (Meteorological Association of Southern Africa -MASA) na alikuwa Makamu Mwenyekiti wa MASA tangu mwaka 2016 hadi Juni 2019. Kitaifa, Dkt. Kijazi amekuwa Mjumbe wa Bodi ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia “Tanzania Commission for Science and Technology (COSTECH)” na Mwenyekiti wa Jopo la Wataalamu la kutoa Ushauri katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania “Tanzania Coffee Research Institute (TACRI)-Technical Advisory Panel (TAP)”, miongoni mwa nafasi nyingine alizo nazo.

Ari na nia ya kutumikia na kusaidia nchi yake hususan katika eneo la utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa jamii ili kukabiliana na athari za hali mbaya ya hewa, ilimfanya Dkt. Kijazi ajiendeleze kielimu kwa kujiunga na masomo ya Shahada ya Sayansi ya Hali ya Hewa (BSc. Meteorology) katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya na kuhitimu mwaka 2000 ; pia alijiendeleza na kujiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili (MSc. in Environmental Science) katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika ya Kusini na kuhitimu mwaka 2003. Katika jitihada hizo hizo, Dkt Kijazi alipata Shahada ya Uzamivu (PhD in Meteorology) katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika ya Kusini mwaka 2009. Dkt. Kijazi amefanya tafiti kadhaa katika eneo la sayasi ya hali ya hewa na amechapisha tafiti hizi katika majarida mbalimbali ya tafiti yanayotambulikana kimataifa (Peer Reviewed Journals).

Mafanikio na mchango wa Dkt. Kijazi katika fani ya hali ya hewa ni wa kupigiwa mfano na heshima kwake na kwa Tanzania pamoja na Jumuiya ya Kimataifa. Mafanikio haya ni pamoja na Tanzania kupitia TMA kupata cheti cha ubora wa kimataifa cha utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga, yaani ISO 9001: 2015 kilichopatikana mwaka 2017 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu katika bara la Afrika kupata cheti hicho kabla ya tarehe 15 Septemba 2018 ambayo ilikuwa ni tarehe ya mwisho ya matumizi ya cheti cha zamani.

Dkt. Kijazi ameongoza uboreshaji wa huduma zaMamlaka yaHali ya Hewa Tanzania kuwa za kisasa zaidi ambapo vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vimefungwa katika maeneo mbalimbali nchini. Hii imechangia katika ubora wa huduma za hali ya hewa kwa wadau mbalimbali na wadau kuendelea kuridhishwa na huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA hapa nchini.

Dkt. Kijazi ameiongoza TMA kwa mafanikiao makubwa ikiwa ni pamoja na kuongoza mchakato wa kuanzishwa Sheria ambayo imeiwezesha TMA kutoka kuwa Wakala hadi kuwa Mamlaka kupitia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 “Tanzania Meteorological Authority Act No. 2 of 2019.” Dkt. Kijazi ameolewa na ni Mama wa watoto watatu.